Chimbuko la WAENDELEE ni fikra, tafakuri na mawazo ya muda mrefu yaliyotokana na majadiliano na mazungumzo kuhusu hali halisi ya maendeleo duni na maisha ya Wirwana na Wairwana. Changamoto zilizopo katika jamii yetu huko Singida, Kielimu, Kiafya, Uduni wa miundombinu ya barabara, Uharibifu wa mazingira, kilimo duni na ufugaji wa mazoea usio na tija.
Mambo haya yalipelekea kupatikana wazo la kuanzisha Group la WhatsApp lijulikanao kama Team Wirwana ambapo wairwana walianza kujadili masuala mbalimbali ya Wairwana mwanzilishi wa kundi hili akiwa ndugu Ramadhani Abeid Ighondo ambaye alikuwa mwenyekiti.
Baada ya majadiliano ndiyo ikakubalika tuanzishe jumuiya ya uwezeshaji na maendeleo (WAENDELEE) ili tuweze kutimiza ndoto zetu kwa kushirikiana na wanajamii walioko Singida na mamlaka mbalimbali. Jumuiya hii ni ya Wanasingida Vijijini walioko sehemu mbalimbali za nchi na dunia kwa ujumla na ni wanataaluma wa fani mbalimbali. Kwa kutumia taaluma hizi tumeamua tuanze kuboresha hali za kimaisha za sehemu tulikotoka.
Malengo Makuu
- Kuendeleza na kukuza uchumi na maendeleo ya watu wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, kuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo kiuchumi, afya, kijamii na kiutamaduni.
- Kusaidia na kuwatambua watu wanaoishi nje ya Singida Vijijini ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
- Kutengeneza umoja na mshikamano baina ya wale waliotoka Singida Vijijini na kuwaunganisha ili waweze kuwekeza katika maendeleo
Malengo Mengineyo
- Kuibua na kutambua fursa zilizopo Singida ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ili ziwaletee wananchi maendeleo
- Kushiriki katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji huko Singida sehemu zenye vyanzo vya maji kama vile Ntambuko.
- Kuhamasisha upatikanaji wa Elimu bora kwa wananchi wetu
- Kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti,kutunza vyanzo vya maji ili kukomesha ukame na hali ya jangwa wirwana.
- Kuhamasisha kilimo cha kisasa na ufugaji bora.
- Kutengeneza mtandao (networking) kwa wale wote ambao wako maeneo tofauti tofauti duniani katika kujenga Singida.
Sisi kama wanajumuiya wa Singida tunaamini jamii yoyote popote pale wanaunganishwa kwa karibu na mazingira halisi waliomo. Shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kiwango kikubwa zinafanyika kutokana na mchanganyiko wa mali asili mbalimbali zilizopo kwenye eneo husika, jiografia ya eneo, hali ya hewa, mabadiliko ya hali za kiasili na tabia mbalimbali za kimazingira. Kwa hiyo mazingira bora yanaboresha uchumi na ustawi wetu wana Singida, tuyalinde yasichafuliwe na kuharibiwa.
