Asasi ya WAENDELEE kwa kushirikiana na serikali ya Wilaya ya Singida, wadau mbalimbali wa mazingira pamoja na wananchi wameadhimisha siku ya upandaji miti kiwilaya.

Maadhimisho hayo yamefanyika kwa kupanda miti pembezoni mwa bwawa la Masoghweda lililopo kata za Mwasauya na Ikhanoda. Miti hiyo imepandwa upande wa kata ya Ikhanoda(Kisisi).

Katika maadhimisho hayo WAENDELEE iliwakilishwa na Mkiti wa Bodi ya WAENDELEE ndugu Joseph Kijeruda na Mkurugenzi wa idara ya mazingira na misitu(WAENDELEE) ndugu Rajabu A. Mumbee. Wakala wa Misitu Tanzania(TFS) waliwakilishwa na ndugu Athuman Hamisi. Serikali ya Wilaya iliwakilishwa na Ndg. Jacob Chibugwa kutoka katika idara ya mazingira ya Wilaya.

Kwa upande wa wenyeji alikuwepo Mtendaji wa kata ya Ikhanoda Ndg. Kiemi Constantine William, Mtendaji wa kijiji cha Mjughuda Ndg. Msafiri, Afisa kilimo na mifugo(kata) Ndg. Msemo Abdallah, mwenyekiti wa kitongoji cha Masoghweda Ndg. Jumanne Njoka pamoja na wananchi.

Zoezi la upandaji miti hasa pembezoni mwa mabwawa yaliyopo Wilayani litaendelea katika msimu wote wa mvua na litakuwa endelevu ili kuyaokoa mabwawa hayo dhidi ya uharibifu wa mazingira pembezoni unaotokana na kilimo kisichozingitia kanuni za utunzaji mazingira ikiwemo na mengineyo.

WAENDELEE ikishirikiana na serikali ya wilaya iligawa miti takribani 11,000 katika taasisi mbalimbali ikiwemo Shule na taasisi za dini kwa ajili ya maadhimisho hayo.

Miti hiyo itaendelea kupandwa kutegemeana na hali ya hewa ya maeneo husika.

Aidha usambazaji wa miti zaidi utaendelea katika maeneo mbalimbali Wilayani katika msimu huu wa mvua.

Kuna miche ya miti takribani laki tano (500,000) inayotakiwa kusambazwa Wilayani.

WAENDELEE inakaribisha wadau mbalimbali katika kutimiza azma hiyo adhimu ya kusambaza na kupanda miti Wilayani.